“Unadhani sijui nini kitatokea?” Simulizi ya mwanafunzi kutoka Mbeya kuhusu sindano zinazolinda moyo wake
Ukurasa mmoja wa kitabu cha kupaka rangi ulimfanya mwanafunzi kutoka Mbeya atusimulie anavyoishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki na kwa nini huwa anarudi kuchomwa sindano hata kama anaziogopa.

Kwenye kipindi cha Colors to Save Hearts katika shule moja jijini Mbeya, Nyanda za Juu Kusini, tulikutana na mwanafunzi ambaye ameishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki tangu akiwa na miaka mitano.
Vipimo vyetu havikuugundua. Alituambia yeye mwenyewe.
Ukurasa aliokuwa anaujua tayari
Kila mtoto aliyekuwepo alipewa kitabu chetu cha kupaka rangi. Kitabu hiki kinaonyesha kwa picha jinsi kuumwa koo kunavyoweza kuleta ugonjwa wa moyo na jinsi ya kuulinda moyo. Ukurasa mmoja unaeleza kwa nini baadhi ya watoto wenye ugonjwa wa moyo wa rumatiki wanahitaji kuchomwa sindano mara kwa mara ili moyo usiendelee kuharibika.

Alipofika kwenye ukurasa huo, akaishia hapo. Hakuhitaji kuelezwa, kwa sababu hayo ndiyo maisha yake kwa miaka mingi. Akaanza kuisimulia timu yetu hadithi yake.
Safari ndefu hadi kujua anaumwa nini
Alipoanza kuumwa, familia yake ilimpeleka hospitali. Aliambiwa ana vidonda vya tumbo akapewa dawa, lakini hakupata nafuu.
Familia yake ikaamua kwenda kwa daktari mwingine. Vipimo zaidi vikaonyesha kwamba ana ugonjwa wa moyo wa rumatiki na akaanza kuchomwa sindano mara kwa mara ili homa ya baridi yabisi isirudi na kuendelea kuuharibu moyo wake.
Anaelewa kwa nini anazihitaji. Lakini alituambia kwamba kadiri siku ya sindano inavyokaribia ndivyo hofu inavyozidi na kwamba baada ya kuchomwa huhisi ganzi.
Kwa wahudumu wa afya, sindano hii ni kinga ya kawaida tu. Kwake yeye, kila sindano inakuja na hofu na usumbufu. Matibabu mazuri ni dawa sahihi na pia ni kuelewa mgonjwa anajisikiaje anapoipata.

Maswali mawili
Akiongea na daktari wetu, aliuliza: “Nikiacha kuchomwa sindano itakuwaje?”
Daktari wetu alimweleza kwamba akiacha, homa ya baridi yabisi inaweza kurudi na kuuharibu zaidi moyo wake.
Akacheka, kisha akajibu: “Unadhani sijui nini kitatokea?”
Kisha akasema: “Nitakufa.”
Hakuwa anauliza ili apate taarifa. Alishajua jibu na bado anaendelea kwenda kuchomwa sindano zake hata kama anaogopa.
Swali lake la pili lilikuwa gumu zaidi kwetu kulijibu. Aliuliza inakuwaje mtu anaenda hospitali na kurudi nyumbani bila mtu yeyote kugundua kuwa ana ugonjwa wa moyo. Hivyo ndivyo ilivyomtokea yeye.
Hadithi yake inatutaka tufanye nini
Kuuzuia mapema. Ugonjwa wa moyo wa rumatiki huanza na maambukizi ya koo yanayosababishwa na bakteria wa streptococcus yasipotibiwa ipasavyo. Maambukizi hayo yanaweza kuleta homa ya baridi yabisi, ambayo huacha makovu kwenye milango ya moyo (valvu). Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema huu ndio ugonjwa wa moyo unaowapata watu wengi zaidi walio chini ya miaka 25, ukiacha magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo. Ndiyo maana Colors to Save Hearts inawafundisha wanafunzi, walimu na wazazi kuchukua hatua mapema mtoto anapoumwa koo.
Kuugundua haraka. Mwanzoni ugonjwa wake wa moyo ulidhaniwa kuwa ni ugonjwa mwingine. Huduma ya kipimo cha echo karibu na wanakoishi watoto na wahudumu wa afya wanaozijua dalili husaidia watoto kupata majibu sahihi tangu mara ya kwanza.
Kufanya matibabu yavumilike na yasikatike. Sindano za penicillin zinazokaa mwilini muda mrefu, ambazo kwa kawaida huchomwa kila baada ya wiki tatu hadi nne, huzuia homa ya baridi yabisi isirudi. Zinaulinda moyo pale tu mtoto anapoendelea kuzipata, mara nyingi kwa miaka mingi. Mtoto anayeiogopa kila sindano anahitaji zaidi ya kuandikiwa dawa: anahitaji kusikilizwa na sindano zisikosekane hata siku moja.
Kuwasikiliza wanaoishi na ugonjwa huu. Anaielewa hali yake kuliko watu wazima wengi wanavyoweza kudhani. Watoto na familia wanaoishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki wanapaswa kushirikishwa katika kupanga huduma zinazowahusu.
Tunamshukuru kwa kutuamini na kutusimulia hadithi yake. Mtoto wako akiumwa koo na asipone, mpeleke kituo cha afya.
Tumechapisha hadithi hii kwa ridhaa ya maandishi ya familia yake. Hatujatumia jina lake.
Habari zaidi
Habari zote
Siku ya Moyo Duniani 2026: zijue dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto
Katika Siku ya Moyo Duniani tunaiomba kila familia, kila mhudumu wa afya na kila kiongozi Tanzania kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto. Vipimo vya mapema hubadilisha maisha ya mtoto.
Soma zaidi
Colors to Save Hearts yazinduliwa Tanzania
The One New Heart Tanzania imezindua Colors to Save Hearts, mradi wa miezi 12 unaolenga kupunguza ugonjwa wa moyo wa rumatiki miongoni mwa watoto wa umri wa kwenda shule, kupitia kutoa elimu, kugundua ugonjwa mapema, kusaidia rufaa na kuimarisha ushirikiano kati ya shule na vituo vya afya.
Soma zaidi
The One New Heart Tanzania Joins the Global Heart Hub
Tuna furaha kuwajulisha kwamba tumejiunga rasmi na Global Heart Hub, muungano wa kwanza duniani wa mashirika ya wagonjwa wa moyo, unaotetea matokeo bora kwa watu wanaoishi na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Soma zaidi