The One New Heart Tanzania
Uelewa · 29 Septemba 2026

Siku ya Moyo Duniani 2026: zijue dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto

Katika Siku ya Moyo Duniani tunaiomba kila familia, kila mhudumu wa afya na kila kiongozi Tanzania kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto. Vipimo vya mapema hubadilisha maisha ya mtoto.

Picha kutoka: Siku ya Moyo Duniani 2026: zijue dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto

Siku ya Moyo Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 29 Septemba. Mwaka huu kampeni ya World Heart Federation inaitwa Don't Miss a Beat: wito wa kutambua dalili za magonjwa ya moyo, kulinda mioyo yetu na kudai hatua kutoka kwa mifumo ya afya. Kama mwanachama wa World Heart Federation na mwanachama mshirika wa Global Heart Hub, The One New Heart Tanzania inaungana na kampeni hii ikiwa na ujumbe mmoja kwa Tanzania: magonjwa ya moyo kwa watoto lazima yagunduliwe mapema.

Magonjwa ya moyo kwa watoto mara nyingi hayagunduliwi

Magonjwa ya moyo si ya watu wazima peke yao. Baadhi ya watoto huzaliwa nayo. Wengine huyapata baada ya maambukizi ya koo yasiyotibiwa kusababisha homa ya baridi yabisi (rheumatic fever), ambayo inaweza kuharibu milango ya moyo maisha yote. Mwanzoni mtoto anaweza kuonekana mzima, au dalili zikadhaniwa kuwa ni magonjwa mengine kama maambukizi ya kifua ya mara kwa mara. Mara nyingi familia inapotafuta msaada, ugonjwa unakuwa tayari umefika hatua ya juu.

Dalili ambazo kila mzazi na mlezi anapaswa kuzifahamu

Kwa watoto wachanga na wadogo

  • Kupumua kwa kasi au kwa shida, hata akiwa amepumzika
  • Kutoka jasho, kuchoka au kuacha kunyonya mara kwa mara
  • Kuongezeka uzito polepole
  • Kupata maambukizi ya kifua mara kwa mara
  • Midomo, ulimi au kucha kuwa na rangi ya bluu

Kwa watoto wakubwa na vijana

  • Kuishiwa pumzi au kuchoka mapema kuliko wenzake wanapocheza au kutembea
  • Maumivu ya kifua, moyo kwenda mbio au kuzimia wakati wa kucheza au kufanya kazi
  • Miguu kuvimba
  • Koo kuuma, kisha baada ya wiki kadhaa homa na viungo kuuma na kuvimba, jambo linaloweza kuwa homa ya baridi yabisi (rheumatic fever)

Hatua za kuchukua

  • Ukiona dalili yoyote kati ya hizi, mpeleke mtoto kituo cha afya na useme wazi kwamba una wasiwasi kuhusu moyo wake. Uliza kama mtoto anahitaji kuchunguzwa moyo, kipimo cha ECG au kipimo cha echo (ultrasound ya moyo).
  • Mhudumu wa afya akimwandikia mtoto antibiotiki kwa ajili ya koo kuuma, mpe dawa hiyo mpaka dozi imalizike. Hii husaidia kuzuia homa ya baridi yabisi na madhara inayoleta kwenye moyo.
  • Hudhuria kila miadi ya kliniki. Mtoto aliyegunduliwa au kutibiwa anahitaji ufuatiliaji wa mara kwa mara, hata akionekana mzima.
  • Hofu au uvumi visichelewesha matibabu. Magonjwa ya moyo ni hali ya kitabibu. Hayasababishwi na laana wala na jambo lolote walilofanya wazazi.
  • Kama mtoto anashindwa kupumua, midomo imekuwa ya bluu au amezimia, mpeleke hospitali iliyo karibu mara moja.

Wahudumu wa afya na viongozi wanaweza kufanya nini

Wahudumu wa afya wanaweza kusikiliza moyo wa mtoto wakati wa kliniki za kawaida za watoto na kutoa rufaa mapema pale wanapoona jambo si la kawaida. Walimu wanaweza kuwajulisha wazazi pale mtoto anapochoka haraka isivyo kawaida au anapokosa shule mara kwa mara kwa sababu ya ugonjwa. Viongozi na wapangaji wa sera wanaweza kuyaweka magonjwa ya moyo kwa watoto katika mipango ya afya ya taifa, ili uchunguzi, vipimo na matibabu vipatikane kwa gharama nafuu na karibu zaidi na nyumbani.

Heart Champion kutoka timu yetu

Pietro Chille, Mkurugenzi Mtendaji wetu, na Dkt. Lioba Joseph wakiwa chumba cha upasuaji

Pietro Chille, Mkurugenzi Mtendaji wetu, na Dkt. Lioba Joseph wakiwa chumba cha upasuaji

Mwaka huu Dkt. Lioba Joseph, daktari wa magonjwa ya ndani (internal medicine) na Mkuu wa Utalii wa Matibabu katika shirika letu, aliteuliwa kuwa Heart Champion. Tunampongeza. Uteuzi wake unatambua kwamba huduma bora za moyo huanza na watu wanaosimama pamoja na wagonjwa na familia zao na kuwasemea.

Jiunge na kampeni

  • Washirikishe ujumbe huu wazazi, walezi na walimu katika jamii yako, ukitumia #WorldHeartDay na #DontMissABeat.
  • Uliza Moyo Guide maswali yako kuhusu afya ya moyo wa mtoto, kwa Kiswahili au Kiingereza.
  • Soma zaidi kuhusu kampeni ya dunia kwenye worldheartday.org.
  • Changia uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto kupitia ukurasa wetu wa kuchangia.

Don't Miss a Beat. Magonjwa ya moyo kwa mtoto yakigunduliwa mapema, mtoto huyo anapata nafasi bora zaidi ya kuishi maisha kamili na yenye afya.