Colors to Save Hearts yazinduliwa Tanzania

The One New Heart Tanzania imezindua Colors to Save Hearts, mradi wa miezi 12 unaolenga kupunguza ugonjwa wa moyo wa rumatiki miongoni mwa watoto wa umri wa kwenda shule, kupitia kutoa elimu, kugundua ugonjwa mapema, kusaidia rufaa na kuimarisha ushirikiano kati ya shule na vituo vya afya.
Mradi huu unafadhiliwa na World Heart Federation kupitia Emerging Leaders Programme yake, ambayo inasaidia juhudi zinazoongozwa na wenyeji katika kukabiliana na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu na kuboresha afya ya moyo.
Kwa nini ugonjwa wa moyo wa rumatiki unatuhusu
Ugonjwa wa moyo wa rumatiki unazuilika. Unatokana na kuharibika kwa milango ya moyo baada ya maambukizi ya koo yanayosababishwa na bakteria wa streptococcus yasipotibiwa, pamoja na homa ya baridi yabisi. Ingawa unazuilika, bado unasababisha maradhi na ulemavu kwa watoto na vijana katika nchi nyingi zenye kipato cha chini na cha kati.
Watoto wengi wenye ugonjwa wa moyo wa rumatiki katika hatua za mwanzo hawaonyeshi dalili za wazi. Kwa sababu hiyo, mara nyingi ugonjwa huu haugunduliki hadi moyo unapokuwa umeshaharibika kwa kiasi kikubwa.
Tafiti zilizofanyika mashuleni hapa Tanzania zimebaini ugonjwa wa moyo wa rumatiki kwa takriban watoto 21-34 kati ya kila 1,000 wa shule za msingi. Matokeo haya yanaonyesha umuhimu wa kuongeza uelewa, kugundua ugonjwa mapema na kutoa rufaa kwa wakati ili watoto wachunguzwe na kutibiwa.
Kuhusu Colors to Save Hearts
Colors to Save Hearts ilianzishwa ili kuziba mapengo katika uelewa na ugunduzi wa mapema wa ugonjwa wa moyo wa rumatiki kwa watoto.
Mradi huu unatumia shule kama mlango wa kuingilia katika kuzuia ugonjwa, kutoa elimu na kugundua mapema, huku ukiimarisha uhusiano kati ya sekta ya elimu na sekta ya afya.
Katika miezi 12 ijayo, mradi utajikita katika:
-
- Kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa moyo wa rumatiki kwa watoto, wazazi, walimu na jamii.
- Kuwafundisha walimu kutambua viashiria na dalili zinazoweza kuhitaji rufaa kwenda vituo vya afya.
- Kuwafundisha wahudumu wa afya jinsi ya kutambua na kuhudumia wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huu.
- Kufanya uchunguzi mashuleni.
- Kuandaa na kusambaza vitabu vya kielimu vya kupaka rangi ili kusaidia kujifunza kuhusu afya ya moyo na ugonjwa wa moyo wa rumatiki.
- Kuimarisha mfumo wa rufaa kati ya shule na vituo vya afya.
Umuhimu wa kutibiwa mapema
Maumivu ya koo yasipotibiwa yanaweza kuharibu moyo wa mtoto.
Kugundua na kutibu mapema maambukizi ya koo yanayosababishwa na bakteria wa streptococcus kunaweza kuzuia homa ya baridi yabisi na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo wa rumatiki. Kwa hiyo, kuongeza uelewa kwa watoto, wazazi, walimu na wahudumu wa afya ni sehemu muhimu ya kuzuia ugonjwa huu.
Kuhusu The One New Heart Tanzania
The One New Heart Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kuboresha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kupitia kutoa elimu, uchunguzi, kusaidia rufaa, kuwezesha upatikanaji wa matibabu na kuimarisha mfumo wa afya. Shirika hili ni mwanachama wa World Heart Federation na mshirika wa Global Heart Hub.
#EarlyTreatmentSavesLives
Habari zaidi
Habari zote
Connecting the Global Discussion to Patients' Experiences in Tanzania
One of the questions arising from the Global Heart Hub Unite Summit 2026 in Dublin is how patient organizations can help create more meaningful opportunities for patients and caregivers to participate in decisions affecting their care.
Soma zaidi
“Unadhani sijui nini kitatokea?” Simulizi ya mwanafunzi kutoka Mbeya kuhusu sindano zinazolinda moyo wake
Ukurasa mmoja wa kitabu cha kupaka rangi ulimfanya mwanafunzi kutoka Mbeya atusimulie anavyoishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki na kwa nini huwa anarudi kuchomwa sindano hata kama anaziogopa.
Soma zaidi
Siku ya Moyo Duniani 2026: zijue dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto
Katika Siku ya Moyo Duniani tunaiomba kila familia, kila mhudumu wa afya na kila kiongozi Tanzania kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto. Vipimo vya mapema hubadilisha maisha ya mtoto.
Soma zaidi