The One New Heart Tanzania kwenye Kongamano la Dunia la Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki huko Perth, Australia
Huko Perth tulieleza tulichojifunza kwenye kazi zetu mashuleni Tanzania: mtoto akigundulika kuwa na ugonjwa wa moyo wa rumatiki, ni lazima apate matibabu ambayo familia yake inaweza kuyamudu na huduma endelevu.

The One New Heart Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuunganisha ugunduzi wa mapema wa ugonjwa wa moyo wa rumatiki na matibabu ambayo familia zinaweza kuyamudu pamoja na huduma endelevu kwa watoto. Hii ni baada ya kushiriki Kongamano la Dunia la Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki lililofanyika Perth, Australia, kuanzia tarehe 11 hadi 14 Novemba 2026.
Shirika liliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Pietro Chille, ambaye aliwasilisha bango (poster) lenye kichwa “Mzigo wa Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki kwa Wanafunzi Tanzania.” Wasilisho hilo lilieleza uzoefu wetu wa kazi mashuleni na changamoto ambazo watoto na familia zao hukutana nazo ili kupata vipimo na matibabu kwa wakati.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa pamoja na World Heart Federation na National Heart Foundation of Australia. Liliwakutanisha wataalamu wa afya, watafiti, watunga sera, wawakilishi wa wagonjwa na watetezi ili kuimarisha juhudi za dunia dhidi ya ugonjwa wa moyo wa rumatiki.
Matokeo makubwa ya kongamano ni kupitishwa kwa Azimio la Perth. Azimio hili linaweka lengo la dunia la kutokomeza homa ya baridi yabisi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki kama matatizo ya afya ya jamii ifikapo mwaka 2040.
Kupeleka uzoefu wa Tanzania kwenye mjadala wa dunia
Kwa The One New Heart Tanzania, kongamano hili lilikuwa nafasi ya kueleza uzoefu kutoka kwenye jamii ambazo watoto bado wako hatarini kupata magonjwa ya moyo yanayozuilika, na ambako kupata matibabu ya kibingwa bado ni changamoto.
Bango letu lilibeba ujumbe mfupi lakini muhimu: Uchunguzi ni mwanzo tu.
Kwenye moja ya kazi zetu za outreach tulikutana na msichana wa miaka 15 mwenye mitral stenosis kali, yaani mlango mmoja wa moyo kuwa mwembamba sana. Ingawa aligundulika miaka mitatu kabla na madaktari walishauri afanyiwe matibabu, familia yake haikuweza kumudu gharama.
Tulipokutana naye, alikuwa anazidi kupata shida ya kupumua. Hali hiyo iliathiri shughuli zake za kila siku na mahudhurio yake shuleni.
Kisa chake kinaonyesha changamoto kubwa hapa Tanzania. Kumgundua mtoto mwenye ugonjwa wa moyo ni muhimu, lakini kugundua peke yake hakuokoi maisha kama familia haiwezi kumudu matibabu yanayotakiwa.
Kwa hiyo wasilisho letu lilisisitiza umuhimu wa kuimarisha safari nzima ya huduma: kuanzia uelewa na uchunguzi, hadi vipimo vya kuthibitisha ugonjwa, rufaa, matibabu ambayo familia zinaweza kuyamudu, kinga ya kuzuia ugonjwa usirudi na ufuatiliaji wa muda mrefu.
Azimio la Perth lina maana gani kwa Tanzania
Azimio la Perth linasisitiza umuhimu wa kuzuia ugonjwa wa moyo wa rumatiki, kurahisisha upatikanaji wa vipimo vya mapema na kuhakikisha watu ambao tayari wanaishi na ugonjwa huu wanapata huduma sahihi bila kukatika.
Linataka programu za kitaifa za kinga ziimarishwe, dawa muhimu za antibiotiki zipatikane kwa uhakika, mifumo ya kufuatilia wagonjwa iboreshwe na uwekezaji kwenye huduma za afya uongezwe. Pia linasisitiza kwamba jamii zinazoathiriwa na ugonjwa huu zishiriki kupanga programu zinazolenga kuzisaidia.
Vipaumbele hivi vinaihusu Tanzania moja kwa moja. Hapa, gharama, uhaba wa huduma za vipimo na ugumu wa kufikia huduma za kibingwa bado vinawaathiri watoto na familia zao.
Pia vinaendana na kazi tunayoendelea nayo kupitia Colors to Save Hearts, programu inayoongeza uelewa wa ugonjwa wa moyo wa rumatiki kwa wanafunzi na jamii, inayohamasisha watu kutafuta huduma za afya mapema na inayoimarisha uhusiano kati ya shule na vituo vya afya.
Kongamano limetukumbusha funzo muhimu la kazi yetu: maendeleo ya kudumu yanahitaji zaidi ya outreach moja moja. Yanahitaji mifumo imara ya afya katika maeneo yetu, jamii zenye uelewa, njia za rufaa zinazoaminika na ushirikiano wa kudumu.
Kutoka kwenye maarifa hadi vitendo
Kwa mujibu wa Azimio la Perth, duniani kote takriban watu milioni 55 wanaishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki na zaidi ya 370,000 hufariki kila mwaka kwa sababu yake.
Pamoja na maendeleo ya sayansi ya tiba, vifo vingi kati ya hivi bado vinaweza kuzuilika.
Akitafakari kuhusu kongamano, Pietro Chille alisisitiza kwamba ugonjwa wa moyo wa rumatiki haupaswi tena kuonekana kama jambo lisiloepukika kwa sababu ya umaskini, hali duni ya maisha au mahali mtu anapoishi.
Changamoto ni kuyageuza maarifa yaliyopo kuwa vitendo kupitia mifumo imara ya afya, uwekezaji endelevu na ushiriki wa kweli wa jamii.
Azimio la Perth pia limeweka ahadi ambazo zitapitiwa kwenye Kongamano la Dunia lijalo mwaka 2029. Hiyo itakuwa nafasi ya kupima hatua zilizopigwa badala ya kurudia ahadi zilezile.
Ahadi yetu
Kama mwanachama wa World Heart Federation, The One New Heart Tanzania itaendelea kushirikiana na taasisi za afya, shule, jamii na wadau ili kuboresha kinga, ugunduzi wa mapema na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini Tanzania.
Kushiriki kwetu Perth kumeonyesha tena umuhimu wa kuunganisha uzoefu wa hapa nyumbani na ushahidi wa kisayansi wa dunia, na kuhakikisha ahadi za kimataifa zinaleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii zilizoathirika zaidi.
Lengo letu si kugundua tu watoto wengi zaidi wanaoishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki. Lengo ni kusaidia kila mtoto anayegundulika apate njia ya kweli ya kufikia huduma anayohitaji.
Safari ya kutokomeza ugonjwa wa moyo wa rumatiki inaanza na kinga, lakini ni lazima pia iwahusishe wale ambao tayari wanaishi na ugonjwa huu na hawawezi kusubiri.
Habari zaidi
Habari zote
Connecting the Global Discussion to Patients' Experiences in Tanzania
One of the questions arising from the Global Heart Hub Unite Summit 2026 in Dublin is how patient organizations can help create more meaningful opportunities for patients and caregivers to participate in decisions affecting their care.
Soma zaidi
“Unadhani sijui nini kitatokea?” Simulizi ya mwanafunzi kutoka Mbeya kuhusu sindano zinazolinda moyo wake
Ukurasa mmoja wa kitabu cha kupaka rangi ulimfanya mwanafunzi kutoka Mbeya atusimulie anavyoishi na ugonjwa wa moyo wa rumatiki na kwa nini huwa anarudi kuchomwa sindano hata kama anaziogopa.
Soma zaidi
Siku ya Moyo Duniani 2026: zijue dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto
Katika Siku ya Moyo Duniani tunaiomba kila familia, kila mhudumu wa afya na kila kiongozi Tanzania kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto. Vipimo vya mapema hubadilisha maisha ya mtoto.
Soma zaidi







